#3.
Maswali matatu ya msingi.

JE! MHOJIWA WANGU ANAELEWA KIKAMILIFU WANACHOSAINI?

Haitoshi kwa mtu kusema 'nakubali' ili habari zao zichapishwe au picha zao kuchukuliwa. Idhini sio halisi kama haijaeleweka kikamilifu.

Kwa sababu tu mtu anakubali kuzungumza au anakubali picha yake kuchukuliwa haimaanishi kwamba anafahamu kikamilifu matokeo yake. Haitoshi kumwambia mtu unachotaka kufanya. Fanya la ziada ili kuhakikisha kuwa mhasiriwa anaelewa hatari na kumuonyesha kuwa ana chaguo halisi. Hasa, wanapaswa kufahamu:

  • Jinsi mchakato wa mahojiano au uchukuaji wa video utafanywa.
  • Ni matukio na mambo gani unapanga kujadili.
  • Nani ataweza kuona ripoti hio na kwa muda gani.

Kupata idhini ni fursa na sio kama kikwazo ambacho kinaitaji kushinda. Ikiwa unayemhoji anafahamu hatari na anakubaliana nawe, utakuwa na mahojiano yenye nguvu.

Kiolezo cha kawaida cha uanahabari cha kupata idhini ya mhojiwa mara nyingi kinahusiana na kuhoji watu mashuhuri. Hawa mara nyingi ni watu wenye elimu ambao wanaelewa sheria zilizowekwa katika mchezo ambao wamezoea. Lengo kuu ni kumfikia na kumfanya mwanasiasa au mfanyabiashara aseme mengi iwezekanavyo, na inapendekezwa iwe hadharani na jina lao linawekwa wazi. 

Ni wazi kuwa sampuli hii haifai wakati unafanya kazi na wachangiaji dhaifu, kwani usawa wa nguvu kati ya mhojiwa na mwanahabari umekuwa kinyume. Kwa kuongezea, wazo la kwanza katika hali ya ukatili wa kingono inapaswa kuwa ulinzi wa kutokujulikana kwa anayehojiwa. Hii inamaanisha kutokuwa na matarajio yoyote kwamba mhasiriwa ana jukumu la kuzungumza na umma. 

Hili linafaa kuwa dhahiri. Kila mwanahabari anajua (au anapaswa) kujua hili. Lakini kwa upande mwingine, mtindo wa kisiasa umekita sana na bado unaweza kuwanasa wanahabari. Ikiwa unaripoti juu ya ukatili wa kingono kwenye migogoro, unahitaji kutulia na uhakikishe kuwa unaanzia mahali tofauti kwa kile kinachoitwa ‘idhini halisi’:

  1. Kwanza, weka kando wazo kwamba idhini inahusu tu kumfikia mtu na kumfanya akubali mahojiano. Sio hivyo. Inahusu kuchunguza jinsi mtu anaweza kujenga msingi salama zaidi wa mahojiano ambao unaandamana na hatari kubwa. Ikiwa mtu atabadilisha mawazo yake na ikawa wazi kuwa hataki kuzungumza, basi chukulia hiyo kama inatosha. Kama ilivyo kwenye majaribio ya kuigiza, inamaanisha kuwa mtu huyo sio mwafaka kwa jukumu hili.
  2. Pili, kupata idhini sio kitendo cha wakati mmoja au utaratibu wa kisheria ambao hufanyika mwanzoni tu mwa mazungumzo. Ni mchakato unaoendelea, na ni mjadala ambapo haki ya kuripoti kwa maelezo fulani – au hata kwenye mazungumzo yote yanaweza kubadilishwa zaidi ya mara moja.

Kamwe usishinikize au kumdanganya mtu kuongea kuhusu maisha ya kibinafsi kama ukatili wa kijinsia. Inapaswa kuwa ni chaguo huru na la kueleweka vizuri.

Ni nani anaweza kutoa idhini? 

Mtu pekee ambaye anaweza kutoa idhini ni yule unayemhoji. Ikiwa unayemhoji ni mtoto mdogo au mtu ambaye kwa namna fulani hana uwezo wa kutoa uamuzi kamili, unaweza kuhitaji pia idhini kutoka kwa mzazi au mlezi.[insert note on minors]

Lakini katika hali yoyote, ikiwa huna idhini halisi kutoka kwa anayehojiwa – huna idhini tu. Idhini kutoka kwa jamaa, wakili wa mtu, mpatanishi au mpatanishi kutoka kwa asasi isiyo ya serikali kuwa ni sawa kufanya mahojiano haikubaliki kama idhini. Maridhiano lazima yawe moja kwa moja na unayemhoji .

Ikiwa unafanya kazi na mkalimani, unahitaji kuhakikisha kuwa mazungumzo baina yake na mhojiwa, ni yale  unadhani yanatakikana. Hii, kama mwandishi wa habari Jina Moore anaelezea, inaweza kuwa tatizo. Inaweza kuhitaji hatua za ziada. Huenda utahitaji kumwambia mkalimani yafuatayo:

“Samahani kujirudia, lakini nataka kuhakikisha lengo langu liko wazi: lengo langu ni hili. Niko hapa kwa sababu… ” Na mkalimani anaposema, “Nimeshamwuliza hivyo,” unajibu, “Ninathamini hilo, lakini sheria za kazi yangu zinahitaji kwamba nimuulize yeye mwenyewe moja kwa moja. Kwa hivyo, nakuomba kutafsiri tena ninachosema ili tuweze kuthibitisha hili tena…” [a

Tofauti za nguvu zinaweza kuwa si wazi na wahasiriwa wanaweza kuwa chini ya shinikizo la kuzungumza wakati sio kwa faida yao. Kama mwanahabari, una jukumu la kufuatilia kwa ndani kujua uwezekano wa kuathirika kabla ya kudhani kuwa mhasiriwa ana chaguo la kweli katika kutoa idhini.

Ikiwa mhojiwa amepitia shambulio hivi majuzi (kama vile dakika, masaa, na labda siku kadhaa) anaweza asiwe tayari kutoa idhini halisi. Kunaweza kuwa na njia ya kuripoti kile kilichotokea kwa kutumia habari za ziada kwa njia ambayo una hakika haitasababisha kutambuliwa kwa mhasiriwa. Lakini ni lazima ufahamu kuwa mtu aliye katika hali kama hiyo hayuko katika nafasi ya kufanya uamuzi kuhusu ikiwa atafutilia mbali haki yake ya kutokujulikana. Hiyo itahitaji muda zaidi baada ya shambulio. Hiyo itaitaji umbali zaidi kutoka eneo la shambulio.

Kufanya kazi na wakalimani

Ikiwa unafanya kazi katika eneo ambalo wewe si mwenyeji, utahitaji uhusiano wa wanahabari na wakalimani wenyeji ambao wanaweza kuzungumza lugha ya hapo na wanafahamu maeneo hayo. Lakini usidhanie kuwa lazima wanafahamu maswala ya kiwewe.

Unahitaji kuhakikisha kuwa kila mkalimani anaelewa kuwa: 

  • Mada inaweza kuwa ngumu kihemko. (Unapaswa pia kuangalia ili kuona ikiwa kuna hatari yoyote kwao au kwa familia zao). 
  • Haipaswi kushinikiza au kutoa vishawishi kwa wahojiwa kuongea.
  • Je, idhini ya kueleweka na mahojiano kuhusu masuala ya kiwewe yanaendeshwa vipi. (Waonyeshe rasilimali kutoka kwa mwongozo huu).
  • Wakati wa mahojiano, wanahabari hawapaswi kushinikiza wahasiriwa katika mambo ya huzuni au kutafuta habari isiyo ya manufaa.

Unapaswa kupanga kwa kina jinsi utakavyofanya mahojiano kabla ya wakati kadri uwezavyo na pia ikiwezekana kufanya mazoezi ya kile utakachofanya. Kuwa na ufahamu kamili juu ya hatari na kanuni za kitamaduni. Uliza mwelekezi wako pia kwa maoni kuhusu namna ya kuendesha mambo na ikiwa wanapata ugumu wa kukufanyia ukalimani. Pindi anakuwa na uaminifu kwako, kazi inakuwa bora zaidi. Unapashwa kuanglia jinsi wanavyoendelea ki binafsi na ikiwa kuna hatari yoyote kwao nafamilia zao.

Ni nini maana ya idhini halisi?

Kwa sababu tu mtu anakubali kuongea, haimaanishi kwamba anaelewa kikamilifu matokeo yake.

Inawezekana kuwa hawafahamu vizuri mchakato, nini utawauliza na jinsi hiyo inaweza kusababisha uchungu na pia nini kitatokea baada ya mahojiano. Cha muhimu ni kuzuia mshangao na chochote kinachoweza kusababisha madhara zaidi mbeleni. Angalia kuwa wewe na anayehojiwa mnaelewa vizuri kuhusu yafuatayo:

  • Nini lengo la mazungumzo
  • Nani atahusika
  • Ikiwa kuna mambo ambayo hayawezi kuzungumziwa kabisa
  • Nani ataona ripoti hiyo (na kwamba inawezekana kupatikana kupitia mtandao mahali popote ulimwenguni)
  • Ikiwa ni video, itapatikana kwa muda gani na itasambazwa vipi
  • Jinsi kutokujulikana kwao kutalindwa
  • Ikiwa kuna uwezekano wa kutambuliwa na kufanyiwa madhara mtandaoni

Ikiwa unatumia picha, ni ada nzuri kumshirikisha mhojiwa katika uamuzi na kuwaonyesha nini watu wengine wataona juu ya maisha yao na jamii wanayoishi. Waandishi wa habari walioripoti juu ya ubakaji wa wanawake wa Yazidi na ISIS walidhani wanawake hao hawatajulikana kwa kuwapiga picha wakiwa wamefunikwa nyuso zao. Lakini wanawake wenyewe waliweza kujitambulisha kupitia macho yao na pia kwa sababu kila mmoja alikwa na mtandio unaombainisha. [tazama #8]

Uzingativu zaidi utahitajika ikiwa, kwa mfano, masuala nyeti kama haya hayajafafanuliwa:

  • Je! video au ripoti ya mwisho itakuwa na sauti za wahalifu, au vikundi vinavyowaunga mkono? Kugundua baada mambo yashafanyika inaweza kuhuzunisha sana. Aliyenusurika  anaweza kuwa na ugumu mkubwa kuelewa kanuni ya ‘haki ya kujibu’ na jinsi mtu yeyote anaweza kuwapa wanyanyasaji nafasi ya kujibu. Ni bora kulielezea hili mapema.
  • Je, kuna matarajio yaliyofichika ambayo hayajashughulikiwa? Je! mhojiwa wako anaamini kuwa kuzungumza na wewe kutaleta msaada wa moja kwa moja kwa jamii? Au ana matarajio kwako kuendelea kumpa msaada wa kisaikolojia au urafiki ambao huwezi kutimiza? [Kuna maelezo zaidi katika #6].
  • Mara nyingi, wanahabari hawafikirii juu ya matokeo ya kisheria ya mazungumzo yao na wahasiriwa wa ukatili wa kijinsia kwenye migogoro. Ikiwa mhojiwa ana nia ya kutafuta haki kortini, basi kuzungumza na wanahabari kunaweza kudhoofisha kesi yake. Unapaswa pia kujua kwamba rekodi zako zote zinaweza kuchukuliwa kuwa ushahidi. 

Mchakato wa kimahakama na hatari ya masimulizi yanayokinzana

Mchakato wa kisheria katika kutafuta haki kwa wahasiriwa wa vurugu wakati mwingine unaweza kuathiriwa na mahojiano mengi. Mwanahabari wa Colombia Jineth Bedoya anaelezea kama ifuatavyo:

Ni moja wapo ya shida kubwa tunayo katika visa vya ukatili wa kingono.

Huko Colombia, sheria inasema kwamba mhasiriwa halazimiki kutoa ushuhuda wake juu ya tukio zaidi ya mara moja. Lakini, wengi wa wahasiriwa wanalazimika kutoa zaidi ya mara nne jambo ambalo linapelekea kutofautiana kwa ushuhuda ambayo mara nyingi husababisha kuzorota kwa michakato ya kimahakama. Athari inakuwa kubwa zaidi ikiwa mhasiriwa ametoa ushuhuda wake kwa vyombo vya habari.

Kwa bahati mbaya, waandishi wa habari wanategemea kutokubaliana kwa ushuhuda ili kupata ile iliyo halisi jambo ambalo husababisha kufungwa kwa mchakato wa sheria.

Vivyo hivyo, masimulizi ya kitendo cha jinai cha ukatili wa kingono, bila kesi, kinasababisha uwasilishaji wa hoja za utetezi kwa wahalifu, ambao mara nyingi hutegemea ushahidi wao juu ya” kukinzana kwa masimulizi”ambayo wahasiriwa wameongea katika mahojiano na chombo cha habari. Waamuzi hawazingatii mazingira ya njia, wakati, na mahali ambapo ushuhuda wa mhasiriwa hutolewa hadharani. Na ni wazi kuwa athari ya kisa ni tofauti katika mahojiano na mwandishi wa habari kuliko na mwanasaikolojia au mtaalamu wa afya.

Jineth Bedoya Lima, ambaye alichangia katika utafiti wetu, alitekwa nyara mara mbili huko Colombia mnamo Mei 2000 na Agosti 2003. Mnamo 2001, alipewa Tuzo ya Courage In Journalism Award kutoka kwa shirika la International Women’s Media Foundation. Pia alishinda tuzo ya ‘Golden Pen of Freedom’ kutoka World Association of Newspapers and News Publishers mnamo 2020. 

Rasilimali za ziada

Jina Moore, mwandishi wa habari wa Amerika anayefanya kazi Afrika Mashariki, ameandika makala mawili muhimu yanayoelezea maswala ya idhini kwa undani zaidi: Mtego wa Ponografia katika jarida la Columbia Journalism Review na pia: Mawazo matano juu ya idhini ya maana katika Uandishi wa Habari za Kiwewe